Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Taifa cha Ulinzi - Tanzania

Chuo cha Taifa cha Ulinzi ni nini?

Chuo cha Taifa cha Ulinzi - Tanzania ni kituo chenye umahiri wa kufanya mafunzo ya Usalama wa Taifa kwa namna ya kipekee na ya kina zaidi. Ni Taasisi mtambuka ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Imeanzishwa na kupewa mamlaka ya kuendesha Kozi ya Mafunzo ya Usalama na Mikakati kwa maafisa wakuu kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama na Utumishi wa umma. Kusudi lake ni kuwajengea watunga sera wa vyombo vya Ulinzi na Serikali uhusiano unaohitajika wa kiuchumi, kisiasa, kijeshi, kisayansi, kimataifa na maarifa ya muundo wa kitaifa ili kuelewa usalama wa kitaifa katika mabadiliko yake ya ndani na nje. Katika mafunzo ya wiki arobaini na saba, washiriki wa Kozi hufunzwa mambo mtambuka nyanja nyingi ambazo huwawezesha kushughulikia ipasavyo changamoto zinazoathiri usalama wa taifa. Chuo cha Taifa cha Ulinzi pia kinatoa fursa kwa maafisa hao wakuu waliochaguliwa kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na hivyo kuwezesha kutathimini kwa jumla matatizo ya kila mmoja, katika amani na vita. Kwa hiyo kozi hii inawajengea uwezo washiriki wa Kozi katika kutunga sera madhubuti katika ngazi ya juu ya kimkakati.